Biashara ya mtandaoni inakuwa kwa kasi. Kila mtu mwenye biashara anatafuta namna ya kuifanya iwe mtandaoni. Kila kitu katika maisha yetu sasa kinageukia mifumo ya kidigitali. Hivyo ni kawaida sana kushuhudia biashara ya vyakula mtandaoni ikikua pia. Ni fursa ambayo ukiwa na nia na dhamira, basi kufanikiwa si kazi ngumu. Kwa nini? Kwa sababu wengi hawaiwekei maanani. Kuna njia nyingi sana za kuuza chakula mtandaoni. 

Hivyo kama umepanga kutumia fursa hii, hizi ni baadhi ya hatua muhimu za kufanya wakati wa kuanzisha biashara vya vyakula mtandaoni

1. Fahamu Vema Sheria ya Uuzaji wa Vyakula

biashara ya vyakula fahamu sheria

Kabla hujafanya chochote, unahitaji kuhakikisha kuwa una uelewa wa kanuni na sheria zinazoongoza uuzaji wa vyakula. Mfano, ni muhimu kujiuliza: Je, vyakula unavyotaka kuuza unaandaa kutoke nyumbani au una sehemu maalum kama mgahawani? Tuseme unataka kutengeneza keki kutokea nyumbani, ni wazi sheria utakazotakiwa kufuata ni tofauti na yule mwenye mgahawa au duka la kuuzia keki. Hivyo kwa ujumla, inatakiwa ujiandae kwa vitu kama:

  • Ukaguzi wa mara kwa mara kutoka mamlaka ya chakula na dawa (TFDA)
  • Kibali cha kuuza vyakula kutoka mamlaka ya TFDA a
  • Leseni halali ya kufanyi biashara
  • Uwezo thabiti wa kuhifadhi vyakula katika hali ya usafi (Majokofu, Makabati ya vyakula n.k)
  • Hakuna wanyama (mbwa/paka) nyumbani au jikoni kwako

Hizi ni baadhi tu. Mwongozo wa sheria na kanuni muhimu za kufungua biashara ya chakula inapatikana kwenye tovuti ya TFDA. Hivyo, soma kwa makini kanuni zote kabla ya kuanza kuuza mtandaoni. Vinginevyo, unaweza ukahatarisha biashara yako na kufungiwa.

2. Chagua Soko na Aina ya Vyakula

Kila mtu anakula. Lakini haimaanishi kila mtu anaweza kuwa mteja wako. Kudhani kuwa kila mtu atapenda chakula unachouza, ni kosa la wajasiriamali wengi wanaochipukia katika biashara ya vyakula mtandaoni. Ukitaka kufanikiwa zaidi, ni lazima uwe na kundi maalum la watu na vyakula unavyouza. Hii itasaidia kurahisisha vitu kama pale utakapotaka kufanya marekebisho ili kukidhi haja za wateja wako.

Chagua aina ya chakula ambacho unaweza kukiandaa vizuri. Kama wewe ni mtaalamu wa keki usipoteze muda wako kuuza ugali. Pili, hakikisha unawatambua wateja wako kufuatana na bei unayouzia. Mfano, kama umeamua kuuza pilau kwa shilingi 20,000 ni lazima ujue mteja wako atakuwa nani na atatoka wapi. Lakini ni muhimu pia kuchagua soko ambalo unaweza kushindana nalo. Kama unaona kuna watu wengi wanatengeneza keki bora kuliko za kwako, basi si jambo baya sana kutafakari zaidi juu ya soko unalotaka kuingia.

3. Tengeneza Jina

biashara ya vyakula tengeneza jina

Baada ya kuhakikisha unajua nini utakachouza na nani utamuuzia, basi itakuwa rahisi sana kwako kutengeneza na kukuza jina lako. Mara nyingi, jina lako litakuwa na kujulikana kutegemeana na chakula unachoouza. Pia,  muhimu kuhakikisha jina linasadifu unachofanya. Watu wanaweza kununua chakula kutoka sehemu yeyote, lakini jina la biashara yako ni muhimu lieleze kwa nini waje kununua kwako. Fikiria, makampuni kama KFC, McDonals au Kahawa Cafe. Ukisikia tu majina yao, unajua wanauza nini. Katika biashara ya vyakula vya mtandaoni, hakikisha unakuza jina la biashara yako  ili watu waweze kukufikia kirahisi. Mfano, kama unauza keki, basi ifike mahali watu wakisema keki wanakuongelea wewe. Ama wakisema biriani wanakutambua kuwa wewe ni bora zaidi.

Kukuza jini kutatokana na mambo mengi kama ubora wa chakula chako, huduma kwa wateja na kitu cha tofuati ambacho hakipo katika biashara nyingine. Kwa mfano, fikiria kama wewe unauza keki na keki zako zinapelekwa kwa wateja na vijana waliovaa suti tu. Ama unauza pizza na pizza zako zinakuwa “delivered” na watu wanaotembea kwa viatu vya matairi. Hii ni mifano tu. La muhimu ni kuhakikisha kuwa kuna utofauti jinsi biashara yako inavyofanyika (business model)

4. Vifungashio na Lebo

Kama bidhaa nyingine yeyote, vifungashio vya vyakula unavyouza mtandaoni ni muhimu sana. Ukiachilia mbali kuambatanisha vitu kama jina la biashara/bidhaa, rangi zinazoakisi biashara yako na nembo, kuna vitu vingi inatakiwa uangalie wakati wa kufunga vyakula vyako.  Vyakula vinatakiwa vifungwe katika hali ya usafi wa hali ya juu. Kama ni chakula ambacho kinahitaji kuhifadhiwa kwenye sehemu yenye ubaridi, basi kifungashio chake lazima kiakisi hilo. Na kama ni vyakula ambavyo haviharibiki kwa haraka, mfano asali, basi hakikisha pia vifungashio vyake vina ubora wa kutosha. Kuna sheria na kanuni za kufunga na kutunza vyakula, hivyo ni muhimu kuzingatia. Pia, kuna kanuni zinazotakiwa kufuatwa wakati wa kuweka lebo katika vifungashio, mfano:

  • Orodha ya viungo vilivyomo
  • Kiwango/uzito
  • Jina na Sehemu ilipo Kampuni
  • Tarehe ya mwisho wa matumizi n.k

Ni muhimu kuhakikisha unatimiza mahitaji ya sheria ili kuepuka usumbufu wakati unaanza kutangaza na kusambaza vyakula vyako mtandaoni.

Jiongeze katika hili. Kama unauza asali basi tafuta kifungashioa ambacho kiko tofauti na vingine. Kama unauza chakula jitofautishe kwa kuweka majonjo yako kwenye vifungashio vyako ili wateja waje kwako.

5. Tangaza Chakula Chako

biashara ya vyakula tangaza chakula

Kutengeneza uhusiano na wateja wako ni nguzo muhimu ya biashsara ya mtandaoni. Kuitafutia  bidhaa yako masoko na kuitangaza, haitakufanya ujulikane tu, bali pia itakusaidia kutengeneza uhusiano wa karibu na wateja wako na kuwafanya wawe sehemu ya biashara  yako. Kuna njia nyingi sana za kutangaza na kufanyia masoko biashra yako ya chakula. Unaweza kutangaza bure kupitia kurasa za mitandao ya kijamii, mfano Facebook and Instagram. Hizi zitakusaidia kutengeneza uhusiano kati yako na wateja wako. Si unajua maoni yao (hasi na chanya) ndio kufanikiwa kwa biashara yako? Hivyo, bila hivi huwezi kujua watu wanapenda, hawapendi au wanaongea nini kuhusu bidhaa yako.

Pia usisite kushiriki katika makongamano ya vyakula ambapo watu tofauti hualikwa kuonja ladha tofauti za vyakula zinazouzwa na wauzaji tofauti. Fanya siku hii kuwa muhimu kuliko zote katika biashara . Andaa chakula chako kwa kiwango cha hali ya juu ili watu wakionja mara moja tu wapate hamu ya kukupata tena. Beba kadi za biashara (business cards) na kuwa tayari kutoa ofa, mfano kupeleka  chakula sehemu yeyote bure kwa wateja wapya.